Na Joseph Ngilisho Arusha
Aliyekuwa mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk John Pima (44) na wenzake wawili mapema leo wamefikishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha wakikabiliwa na kesi nyingine ya uhujumu uchumi yenye mashtaka sita ikiwemo mawili ya utakatishaji fedha.
Dkt Pima na wenzake leo walifika mahakamano kwa ajili ya kuomba dhamana lakini waligonga mwamba baada ya kujikuta wakisomewa mashtaka mengine ya utakatishaji fedha haramu ambayo kisheria hayana dhamana.
Wshatakiwa wengine waliosomewa mashtaka mengine ni Mariam Mshana (40), aliyekuwa mkuu wa idara ya fedha ya halmashauri hiyo na Innocent Maduhu (40) aliyekuwa mkuu wa idara ya mipango ya uchumi.
Mbali na watuhumiwa hao, wengine ni Nuru Ginana na Alex Daniel ambao walikuwa wachumi katika jiji hilo, nao walifikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kukamilisha dhamana ambapo kupitia mawakili wao waliieleza mahakama hiyo kuwa hawajakamilisha masharti ya dhamana.
Katika kesi hiyo Jamhuri inawakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janeth Sekule, Wakili wa Serikali, Charles Kagilwa na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Richard Jacopiyo huku washtakiwa hao wakiwakilishwa na Mawakili Valentino Nyalu na Sabato Ngogo.
Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5/2022, washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa sita ambapo kosa la kwanza linalowakabili ni ufujaji na ubadhirifu wa Sh103 milioni, kosa la pili na la tatu ni kutumia nyaraka kwa malengo ya kumdanganya mwajiri.
Kosa la tano linalomkabili Maduhu ni utakatishaji fedha huku la sita likiwa utakatishaji ambalo linawakabili wote watatu.
Washtakiwa wote walikana kutenda makosa hayo na upande wa Jamhuri ulieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika .
Hakimu Mwakisu aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 5, mwaka huu na washtakiwa walirudishwa mahabusu katika gereza kuu la Arusha.
Wiki iliyopita Pima akiwa na wenzake wanne akiwemo Mariamu Mshana{43} mweka hazina Jiji,Innocent Maduhu{40} Nuru Saqware na Alex Tihema walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka manne ikiwemo la Uhujumu Uchumi akidaiwa kumdanganya mwajiri wake na kujipatia kiasi cha shilingi milioni 67 wakati wakijua wazi kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Ends...
0 Comments