Benki ya Dunia (WB) imetoa mkopo wa masharti nafuu wa zaidi ya Sh210 bilioni kwa Serikali kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya mahakama katika mwaka wa fedha 2022/2023.
Akizungumza leo Jumatano Juni 29,2022 wakati akifungua baraza la wafanyakazi, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma alisema lengo la mkopo huo ni kuimarisha miundombinu ya mahakama ili waweze kufanya kazi katika mazingira mazuri.
“Hivi karibuni Serikali ya Tanzania mkopo wa gharama nafuu wa Dola za Marekani milioni 90 ambazo ni zaidi ya Sh210 bilioni kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya mahakama kwa mwaka ujao wa fedha (2022/2023),” alisema.
Alisema Wizara ya Fedha na Mipango imekuwa ikitoa fedha kwa wakati katika miradi ya maendeleo inayoendelea na kwamba hata kama kuna changamoto mawasiliano yamekuwa yakifanyika kwa haraka.
Aliahidi Serikali kuwa watasimamia vizuri fedha hizo kwa sababu wakizipata zinawasaidia katika shughuli zetu za utoaji wa haki.
“Wafanyakazi na watumishi nawaomba tuhakikishe tunatimiza wajibu wetu kuwa mkopo huu unatumika katika kusogeza haki kwa miaka mingi ijayo,” alisema Profesa Jumaa.
Alisema pia ni jukumu lao kuhakikisha majengo mazuri yanaendana na huduma bora kutoka katika majengo hayo.
Profesa Juma alisema kuwa mpango wa kuboresha miundombinu ni endelevu na kwamba umetajwa hata katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel alisema hadi kufikia Machi mwaka 2022 walikuwa na watumishi 5,808 lakini watendaji wanaohitajika ni 10,352 na kuna upungufu wa watumishi 4,544.
0 Comments